Afisa Tarafa wa Pangani Mjini Ndugu Heliswida Majula akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Pangani leo Februari 17, 2024 amezindua kampeni ya kitaifa ya utoaji wa Chanjo ya Surua na Rubella katika ofisi ya Kata ya Pangani Magharibi Wilayani Pangani, ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa hamasa ya utekelezaji wa kampeni hiyo.
Kampeni hiyo iliyoanza siku ya Tarehe 15, Februari 2024 na itaendelea hadi 19 Februari 2024, kwa Watoto wote wenye umri kuanzia miezi 9 hadi miaka 5.
Ndg Heliswida Majula ameendelea kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kupambania Afya za Wananchi hivyo tuzidi kumuunga mkono kwa kuwaleta watoto wapate chanjo hizi muhimu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji ndg Juma Mbwela ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha Wazazi na Walezi kuwapeleka watoto wao katika vituo vyote vya Afya, zahanati, na maeneo yote yanayotoa chanjo hiyo ili kujikinga na magonjwa hayo ambayo ni hatari kwa Afya.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Ramadhani Hussein amesema kuwa tangu kuanza kwa kampeni hiyo Februari 15, 2024 tayari chanjo hizo zilishasambazwa kwenye vituo vyote vya Afya, pamoja na Zahanati ili kuwafikia walengwa hao.
Ifahamike kuwa ugonjwa wa Surua na Rubella ni aina ya magonjwa ambayo husababishwa na virusi vinavyoenea kwa njia ya hewa na kuleta madhara kwa makubwa kwa watoto ambao hawajapata chanjo.
Pangani District Council
Sanduku la Posta: 89 Pangani -Tanga
Namba ya Mezani: +255 (0) 27 2630058
Namba ya simu: 0658100588/062289307
Barua Pepe : ded@panganidc.go.tz
Hakimiliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya Pangani .Haki Zote Zimehifadhiwa