Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Pangani yaiomba Serikali kutafuta ufumbuzi wa kudumu tatizo la kukatika kwa Umeme mara kwa mara Wilayani Pangani.
Yamesemwa hayo leo tarehe 30, Aprili 2025, kwa niaba ya Wananchi na Mh Akida Bahorera Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani katika Mkutano wa Baraza la Madiwani Robo ya Tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Mh Bahorera ameeleza kwamba Serikali Chini ya usimamizi wa Mh Rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya maendeleo makubwa sana kwa Wilaya ya Pangani katika Sekta zote, Elimu, Afya, Miundombinu, Kilimo,Mifugo na Uvuvi lakini bado kuna hilo tatizo la Umeme kutokuwa na uhakika hali inayopelekea Uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Pangani kutoimarika kwa sababu asilimia kubwa ya wananchi wa Pangani uchumi wao unategemea zaidi Sekta ya Uvuvi ambapo matumizi ya Umeme ni lazima.
aidha ameeleza kwamba Wananchi wa Pangani waliambiwa tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara linatokana na miundombinu kuwa chakavu, kuwa na kituo kimoja cha kupoozea pamoja na njia ya umeme kuwa na miti, lakini Serikali ilitoa fedha kutatua hayo yote ambapo kuhusu nguzo Serikali ilileta nguzo za Zege, kuhusu Njia ya umeme ilitoa fedha za kutosha kusafisha njia kubwa ya umeme kuhakikisha nguzo zinakuwa salama muda wote na kuhusu Vituo vya kupoozea Serikali ilielekeza Pangani kupata umeme kupitia Muheza na Tanga Mjini.
Mhe Bahorera ameeleza kwamba kutokana na jitihada hizo zilizofanywa na Serikali wananchi hawaelewi ni kwanini bado Wilaya inaendelea kuwa na tatizo la Umeme kwa kiasi hicho.
Aidha mhe Bahorera ameiomba Serikali kufuatilia kwa karibu changamoto hiyo na kuhamasisha uwajibikaji na hatua stahiki kwa watendaji wachache wasiowajibika ambao kwa Uzembe wao wanaisababishia Serikali kuendelea kulalamikiwa na Wananchi na huku Wananchi kuendelea kupata hasara katika shughuli zao za kujikwamua kiuchumi wanazofanya.
Pangani District Council
Sanduku la Posta: 89 Pangani -Tanga
Namba ya Mezani: +255 (0) 27 2630058
Namba ya simu: 0658100588/062289307
Barua Pepe : ded@panganidc.go.tz
Hakimiliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya Pangani .Haki Zote Zimehifadhiwa