Katibu Tawala Wilaya ya Pangani Bi. Ester Gama akiambatana na Afisa Elimu Msingi ndg Juma Mbwela, wamewahimiza Wanafunzi walioripoti na walioandikishwa kuzingatia masomo yao.
Hayo yamefanyika leo 9 Januari 2024 wakati wa ukaguzi wa Uripoti na Uandikishwaji wa Wanafunzi katika Shule mbalimbali Wilayani Pangani.
Akizungumza na Wanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Tongani ndg Gama amewataka Wanafunzi hao kushirikiana wao kwa wao katika masomo, na waendelee kuelekezana ili waweze kutimiza ndoto zao.
"Mimi niwaombe watoto wangu ili muweze kutimiza ndoto zenu jitahidini sana kuzingatia masomo na kuelekezana ninyi kwa ninyi, wewe unaejua hesabu kuwa mwalimu kwa mwenzako ili wote mfanye vizuri".
Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi ndg Juma Mbwela amewataka Walimu wazidishe ubunifu zaidi katika kuwafundisha wanafunzi ili waweze kupata matokeo mazuri.
Kaimu mkuu wa shule hiyo ndg Valerian Nestory Godfrey ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na uongozi mzima wa Halmashauri ya Pangani kwa kuboresha mazingira mazuri ya Elimu.
"Kiukweli Uripoti na Uandikishaji wa Wanafunzi unaendelea vizuri toka jana tulipofungua Shule na Asilimia kubwa ya Wanafunzi wamekwisha ripoti, tayari wanaendelea na masomo yao,lakini pia tunaendelea kutoa woto kwa wazazi kuendelea kuwaleta watoto kujiandikisha".
Ikiwa ni mwendelezo wa Uandikishaji na uripoti wa Wanafunzi Katibu Tawala Wilaya amepata nafasi ya kuzitembelea shule mbalimbali ikiwemo Shule ya Sekondari Tongani Shule ya Msingi Mkalamo, Shule ya msingi Mkwaja,Shule ya Sekondari Mkwaja,Shule ya Msingi kipumbwi, Shule ya Msingi Kipumbwi Pwani, pamoja na Shule ya Sekondari Kipumbwi.
Pangani District Council
Sanduku la Posta: 89 Pangani -Tanga
Namba ya Mezani: +255 (0) 27 2630058
Namba ya simu: 0658100588/062289307
Barua Pepe : ded@panganidc.go.tz
Hakimiliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya Pangani .Haki Zote Zimehifadhiwa