Na. James K. Mwanamyoto OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Maafisa Habari Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Seriksali za Mitaa kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika maeneo yao ya kazi.
Waziri Mchengerwa ametoa wito huo leo, wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Habari wa Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Ofisi ya Rais-TAMISEMI kinachofanyika katika Ukumbi wa Jiji la Dodoma uliopo kwenye Mji wa Serikali Mtumba mkoani Dodoma.
“Mmebeba dhamana kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi hivyo msiwaache watanzania walishwe habari potofu” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa amesema kuwa, Maafisa Habari nchini ni rasilimaliwatu muhimu hivyo wakitambua wajibu wao na kujiimarisha kiutendaji ni wazi kuwa wananchi watapata taarifa sahihi kwa wakati.
“Iwapo kila mmoja wenu akiwa mzalendo na kutambua wajibu wake, habari mtakazozitoa ndio zitaaminiwa na kupokelewa na watanzania kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ambayo imeshamiri hivisasa,” Waziri Mchengerwa amehimiza.
Waziri mchengerwa amesema, ana amini kwamba maafisa habari waliopo wana weledi na ujuzi unaowawezesha kutoa taarifa sahihi zenye tija kwa wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Sanjari na hilo, Waziri Mchengerwa ameelekeza Maafisa Habari wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa washiriki kwenye ziara za viongozi ili wapate uelewa utakaowawezesha kutangaza kwa ufanisi mafanikio ya Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha, Waziri Mchengerwa amewaelekeza waajiri katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha Maafisa Habari wanaokaimu ukuu wa vitengo ambao wana sifa, wapewe vitengo ili waweze kutekeleza kikamilifu jukumu la kuuhabarisha umma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi zao ikiwa ni pamoja na kutangaza mafanikio yaliyopatikana kwenye eneo la utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambalo limepewa kipaumbele na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Pangani District Council
Sanduku la Posta: 89 Pangani -Tanga
Namba ya Mezani: +255 (0) 27 2630058
Namba ya simu: 0658100588/062289307
Barua Pepe : ded@panganidc.go.tz
Hakimiliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya Pangani .Haki Zote Zimehifadhiwa