Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), imetekeleza mradi wa maji safi na salama wenye thamani ya shilingi milioni 500 katika Kijiji cha Tungamaa, wilayani Pangani mkoani Tanga, ambapo zaidi ya kaya 600 zimeanza kunufaika na huduma hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian, Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Gift Msuya, alisema mradi huo umeongeza kiwango cha upatikanaji wa maji wilayani humo hadi kufikia asilimia 86 kwa vijiji na asilimia 76 kwa maeneo ya mijini.
“Tunatarajia kufikia lengo la asilimia 100 ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa wilaya ya Pangani ifikapo Desemba mwaka huu, kama ilivyo katika mipango ya serikali ya awamu ya sita,” alisema Msuya.
Alisema serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji kwa kasi ili kuhakikisha wananchi, hasa wa vijijini, wanapata huduma hiyo kwa ukaribu zaidi, ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Maji inayotaka mwananchi kutotembea zaidi ya mita 400 kufuata huduma ya maji.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga, Mhandisi Upendo Lugongo, alisema utekelezaji wa mradi huo umezingatia viwango na ubora unaostahili, na umeleta mafanikio makubwa katika kuboresha maisha ya wananchi wa Tungamaa.
“Kwa sasa wananchi wameanza kupata maji moja kwa moja majumbani mwao, jambo ambalo limepunguza adha ya kutumia muda mwingi na nguvu kutafuta maji mbali na makazi yao,” alisema Lugongo.
Mradi huo ni sehemu ya jitihada za serikali za kuondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji vijijini, na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla kupitia utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya taifa.
Pangani District Council
Sanduku la Posta: 89 Pangani -Tanga
Namba ya Mezani: +255 (0) 27 2630058
Namba ya simu: 0658100588/062289307
Barua Pepe : ded@panganidc.go.tz
Hakimiliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya Pangani .Haki Zote Zimehifadhiwa