Madiwani Wajengewa Uwezo kwa Ajili ya Kuimarisha Maendeleo ya Pangani.

Wananchi wa Wilaya ya Pangani wanatarajiwa kunufaika na huduma bora pamoja na kuimarika kwa maendeleo kufuatia mafunzo elekezi ya Waheshimiwa Madiwani yaliyoanza leo Januari 26, 2026, Ukumbi wa Usagara jijini Tanga.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamefunguliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Dadi Kolimba, ambaye alisisitiza umuhimu wa madiwani kusimamia vyema rasilimali za umma, kupanga na kutekeleza bajeti kwa ufanisi, pamoja na kuzingatia maadili ya uongozi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mhe. Kolimba alibainisha kuwa madiwani ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi, na kwamba mshikamano kati ya madiwani na wataalamu wa halmashauri ni msingi imara wa kufanikisha maendeleo endelevu kwa wananchi.
“Serikali imeona umuhimu wa kuwajengea uwezo Waheshimiwa Madiwani kupitia mafunzo kwenye mada mbalimbali, ikiwemo uongozi na utawala bora, usimamizi wa maendeleo bila kukiuka sheria na taratibu, usimamizi na udhibiti wa fedha katika mamlaka za Serikali za Mitaa, pamoja na usimamizi wa ardhi,” alisema.

Wananchi wanatarajia kuona matokeo chanya ya mafunzo hayo kupitia uboreshaji wa huduma za elimu, afya, maji na miundombinu.

Mafunzo hayo yaliwakutanisha Waheshimiwa Madiwani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tanga na Halmashauri ya Wilaya ya Pangani.
Pangani District Council
Sanduku la Posta: 89 Pangani -Tanga
Namba ya Mezani: +255 (0) 27 2630058
Namba ya simu: 0658100588/062289307
Barua Pepe : ded@panganidc.go.tz
Hakimiliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya Pangani .Haki Zote Zimehifadhiwa