Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Lameck Nchemba, ameonesha kuridhishwa na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa daraja la kisasa katika Mto Pangani, lililopo wilayani Pangani mkoani Tanga.

Akizungumza leo, tarehe 15 Februari 2026, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Mheshimiwa Nchemba amesema kuwa ujenzi wa daraja hilo ni ishara ya mafanikio makubwa ya uongozi wa Serikali katika kuimarisha miundombinu ya kisasa nchini.

Alisisitiza kuwa kwa miaka mingi, Watanzania walizoea kuona madaraja ya kiwango hicho yakijengwa katika mataifa yaliyoendelea kama China, Japani na Korea Kusini, lakini sasa Tanzania inaandika historia yake kwa kujenga miundombinu ya kisasa yenye viwango vya kimataifa ndani ya mipaka yake.

“Hapo awali, madaraja ya aina hii tulikuwa tunayashuhudia katika nchi zilizoendelea, lakini leo daraja hili linajengwa hapa Pangani. Huu ni ushahidi wa uongozi wenye maono, unaoacha alama ya kudumu na urithi utakaoendelea kukumbukwa na vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Mheshimiwa Nchemba.

Aliongeza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutachochea ukuaji wa uchumi, kurahisisha usafiri na usafirishaji, pamoja na kuimarisha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa Pangani na maeneo ya jirani.
Pangani District Council
Sanduku la Posta: 89 Pangani -Tanga
Namba ya Mezani: +255 (0) 27 2630058
Namba ya simu: 0658100588/062289307
Barua Pepe : ded@panganidc.go.tz
Hakimiliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya Pangani .Haki Zote Zimehifadhiwa