Wananchi wa Kijiji cha Mikinguni, Wilaya ya Pangani, wanatarajiwa kuanza kunufaika na huduma za afya hivi karibuni baada ya Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama kwa kipindi cha Juni hadi Desemba 2025.

Ziara hiyo iliyofanyika leo, tarehe 9 Februari 2026, imelenga kukagua ukamilishaji wa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mikinguni, ambapo imebainika kuwa miundombinu ya zahanati hiyo tayari imekamilika.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Chama Wilaya ya Pangani, Mheshimiwa Abdallah Mahmoud, amepongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo na kueleza kuridhishwa kwake na hatua iliyofikiwa.

Aidha, amewahimiza wahusika kuhakikisha kazi chache zilizosalia ikiwemo uwekaji wa vifaa tiba na upangaji wa watumishi wa afya zinakamilika kwa wakati ili zahanati ianze kutoa huduma haraka iwezekanavyo.
“Wananchi wamekuwa na kero ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya. Kukamilika kwa zahanati hii ni hatua kubwa ya kusogeza huduma karibu na wananchi,” alisema Mheshimiwa Abdallah.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Wakili Agape Fue ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutapunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu, hasa kwa akina mama wajawazito, watoto na wazee.
Kwa kukamilika kwa miundombinu, serikali na viongozi wa chama wamehakikishia wananchi kuwa taratibu za mwisho zinaendelea ili zahanati hiyo ianze rasmi kutoa huduma katika muda mfupi ujao.
Pangani District Council
Sanduku la Posta: 89 Pangani -Tanga
Namba ya Mezani: +255 (0) 27 2630058
Namba ya simu: 0658100588/062289307
Barua Pepe : ded@panganidc.go.tz
Hakimiliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya Pangani .Haki Zote Zimehifadhiwa