Pangani, 6 Februari 2026
Halmashauri ya Wilaya ya Pangani kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wizara ya Nishati pamoja na wadau wa mazingira wakiwemo UNCDF na European Union, imetoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, katika tukio lililofanyika leo katika Soko Kuu la Pangani.

Katika zoezi hilo, wananchi walipatiwa elimu kuhusu faida za kutumia majiko ya kisasa ya umeme, ambapo walionyeshwa kwa vitendo jinsi majiko hayo yanavyoweza kupunguza gharama za kupikia ikilinganishwa na matumizi ya mkaa au gesi.

Wawezeshaji walieleza kuwa matumizi ya nishati safi si tu yanaokoa gharama kwa kaya, bali pia yanachangia kulinda afya za watumiaji na mazingira kwa ujumla.
Aidha, programu hiyo iliambatana na hamasa mbalimbali ikiwemo maswali na majibu kuhusu nishati safi ya kupikia, ambapo washiriki walioweza kujibu kwa usahihi walipatiwa zawadi kama njia ya kuhamasisha uelewa na ushiriki wa wananchi.
Juhudi hizi zinaonesha dhamira ya serikali na wadau wake katika kuhakikisha jamii inahamia kwenye matumizi ya nishati safi na salama, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kupunguza matumizi ya nishati chafu na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Pangani District Council
Sanduku la Posta: 89 Pangani -Tanga
Namba ya Mezani: +255 (0) 27 2630058
Namba ya simu: 0658100588/062289307
Barua Pepe : ded@panganidc.go.tz
Hakimiliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya Pangani .Haki Zote Zimehifadhiwa