WAFUGAJI WAHIMIZWA KUCHANJA MIFUGO YAO, KIPINDI CHA CHANJO.
Pangani_ Tanga.
Hayo yamefanyika leo tarehe 2 Januari 2025, katika maeneo mbalimbali wilayani Pangani, ikiwemo kata ya Ubangaa pamoja na kijiji cha Langoni kilichopo kata ya Tungamaa.
Hamasa hiyo imejumuisha timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani ikiambatana na mwenyekiti wa wafugaji mkoa wa Tanga ambao wameendelea na hamasa kwa wananchi juu ya kampeni ya utoaji wa chanjo na uchanjaji wa mifugo Nchi nzima inayotarajiwa kufanyika Januari 2025.
Akizungumza katika kikao hicho afisa mifugo wilaya ya Pangani ndg Daud Mwaushanga amesema kuwa lengo la kukutana na wananchi ni kutoa hamasa ya Chanjo ya Mifugo inayotarajiwa kutolewa kwa Wafugaji, wote Pangani.
" Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatarajia kuendesha kampeni ya utoaji wa chanjo na uchanjaji wa mifugo Nchi nzima kuanzia Januari 2025, hivyo ni jukumu la kila mfugaji kuhakikisha mifugo yote inachanjwa ili kupata mifugo iliyobora. Alibainisha.
Aidha ameongeza kuwa chanjo hii itatolewa kwa magonjwa aina tatu Kideli, Sotoka na Homa ya Mapafu kwa mifugo ikiwemo Ng'ombe, mbuzi pamoja na kuku, na itatolewa kupitia ruzuku ya Serikali na kushirikiana na wananchi kwa muda wa miaka mitano.
Kwa upande wake Daktari wa mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani ndg David Lyimo amesema kuwa ni vizuri kujiandaa juu ya zoezi hilo, kuhakikisha linafanyika, hivyo ni jukumu letu wafugaji kuhakikisha tunafuatilia kwa karibu mifugo yetu ili kutokomeza magonjwa mbalimbali kwa mifugo yetu.
Pangani District Council
Sanduku la Posta: 89 Pangani -Tanga
Namba ya Mezani: +255 (0) 27 2630058
Namba ya simu: 0658100588/062289307
Barua Pepe : ded@panganidc.go.tz
Hakimiliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya Pangani .Haki Zote Zimehifadhiwa